Athari mbaya za mitandao ya kijamii kwa watoto na mabarobaro
Sote tunakumbuka namna
ambavyo, katika miaka iliyopita, tulikuwa tukisikia zauti zilizojaa furaha za
watoto wakicheza mitaani. Watoto wakiwa na nyuso zenye bashasha na msisimko
mkubwa walikuwa wakikimbizana huku na kule wakicheza michezo mbali mbali.
Lakini katika zama zetu hizi, ongezeko la kasi la teknolojia za kisasa ni jambo
ambalo limepeplekea kupungua kwa kiasi kikubwa harakati hizo za watoto
wakicheza nje ya nyumba zao ambapo miili yao ilikuwa ikipata mazoezi na kuwa na
afya bora. Ulimwengu wa leo ni wa kimashine na umezungukwa na teknolojia
mpya za kisasa na hivyo kuwapokonya watoto zile lahadha tulizokuwa nazo miaka
ya nyuma ambapo watoto walitumia wakati wao wa mapumziko wakiwa katika viwanja
vya mitaa wakicheza michezo kama vile mpira, kukimbizana n.k. Kutokana na
kuibuka anuai ya teknolojia za michezo ya kisasa ya kikompyuta, watoto wa leo
hufadhilisha zaidi kupitisha wakati wao wakiwa mbele ya kompyuta au kutumia
vyombo mbali mbali vya kidijitali. Watoto hawa huinukia na kuishi katika
mazingira ya kintaneti kuliko wakati mwingine wowote, na hivyo tunaweza kuwaita
watoto wa zama hizi kuwa ni kizazi cha intaneti.
Pamoja na kuwa hatuwezi
kupinga kuwepo faida nyingi za teknolojia za kisasa na intaneti katika
kurahisisha maisha na mawailisano ya wanadamu, lakini hatupaswi kutekwa na
teknolojia hizo.
Tunapaswa kuwa
waangalifu na tusiache hizo teknolojia za kisasa za habari na mawailisnao
ziharibu dafina ya maadili bora, mahaba ya kifamilia na mahusiano mema ya
mwanadamu. Yamkini mwanzoni ikawa ni ajabu kwetu kuona mtoto wa miaka miwili au
minne akivutiwa na suhula za kisasa za mawasiliano. Tunaona namna watoto wenye
umri wa chini wanavyotumia teknolojia hizi kirahisi. Hatua kwa hatua tunafahamu
ukweli kuwa teknolojia mpya za kisasa ni kati ya bidhaa zinazopendwa zaidi na
watoto wa leo.
Kutokana na kuwepo
wakati wa mapumziko baada ya shule, tunaona watoto wakiwa wametekwa na
teknolojia za kisasa. Wao hupitisha wakati wao mwingi wakicheza michezo ya
kidijitali huku wakivutiwa na utumizi wa intaneti. Hali kadhalika mabarobaro
nao hutumia intaneti na mitandao ya kijamii kama njia ya kustarehe na kuwa na
uhusiano na wenzao.
Ingawa mabarobaro hupata
na kuimarisha maarifa na elimu yao kupitia intaneti sambamba na kuzijua
staarabu na tamaduni mbali mbali kutokana na kutokuwepo mipaka ya kijiografia
katika intaneti, lakini utumizi usio sahihi wa teknolojia ya habari na
mawasiliano au technohama huwa na matokeo mabaya na hatari sana. Ukweli ni kuwa
katika dunia yetu ya leo, intaneti imeweza kujipenyeza katika nyumba zetu na
katika maisha binafsi na kuwa na taathira isiyoweza kuaminika katika thamani na
itikadi za wanaoitumia.
Kutokana na mvuto
maalumu, mitandoa ya kijamii hupelekea watumizi kumalizia muda wao mwingi
katika kompyuta au chochote kilichounganishwa na intaneti kama vile simu
za mkononi. Sifa maalumu ya mitandao hii ya kijamii ni kuwa ni mipana na iliyo
na suhula na uwezo mkubwa wa kuboresha mawasiliano baina ya marafiki na makundi
mbali mbali ya watumizi wa intaneti. Kutokuwepo vizingiti vya zama na mahala
katika mawasiliano baina ya walio katika intaneti na uwezo wa kuwa online
wakati wote ni jambo ambalo hupelekea watoto na mabarobaro kumalizia wakati wao
mwingi katika mitandao hii ya kijamii.
Utumizi wa muda mrefu wa
intaneti baadhi ya wakati hupelekea mtumizi kufungamana sana na njia hiyo ya
mawasiliano na hilo huibua uraibu wa intaneti. Hali kama hii ikijitokeza,
watoto na mabarobaro hukumbwa na matatizo kama vile ukosefu wa usingizi,
uchovu, unene na maradhi yanayoambatana na hali hiyo na hatimaye wengine
hudhoofika kielimu.
Zama za ubarobaro huwa
ni kipindi ambacho utambulisho na shakhsia huibuka na hivyo ni kipindi muhimu
sana kwa mabarobaro. Katika zama hizo mabarobaro hujitahidi kunufaika na
mafundisho na uzoefu wa watu waliofanikiwa maishani ili nao waweze kuwaiga na
kujiandalia nafasi yao katika jamii. Kwa hivyo katika kipindi hicho mabarobaro
na vijana hujitahidi kuwa na uhusiano na watu wengi wasio katika familia zao.
Katika zama zilizopita kulikuwa na nukta ambazo zilikuwa na taathira katika
kuunda utambulisho wa mabarobaro na hilo lilitegemea itikadi na thamani za
kifamilia, mazingira ya shule na pia kundi la marafiki. Lakini kijana na
barobaro wa leo anakumbana na kila aina ya itikadi, tamaduni na thamani. Katika
hali kama hii, barobobaro au kijana hukumbwa na mfadhaiko na vishawishi vingi
wakati wa kuchagua ni njia ipi aifuate katika jamii. Ili kukabiliana na
daghadagha hii, mabarobaro hujaribu kuingia katika maeneo ambayo watahisi
kuwepo usalama zaidi. Katika mazingira hayo, huwa wanaweza kubainisha mitazamo
na itikadi zao bila kuwa na woga na hapo ndipo utambulisho wao huanza kuibuka
hatua kwa hatua. Lakini tatizo sugu ni kuwa katika mazingira ya intaneti,
barobaro huwa hawezi kupapta utambulisho unaofaa kwani yamkini baadhi ya walio
katika mitandao ya kijamii wakawa na utambulisho bandia huku wakijaribu
kuwatwisha wengine mtindo potovu wa kimaisha hasa kutoka nchi za Magharibi.
Tunaona namna katika mitandao ya kijamii kunaenezwa thamani na tamaduni ambazo
zinaenda kinyume kabisa na misingi ya familia na jamii bora. Katika hali kama
hiyo barobaro hujipata katika njia panda ya ima kuchagua kudumisha itikadi zake
za kidini na kifamilia au kuchukua vigezo potovu katika mitandao ya kijamii.
Katika hali kama hii mabarobaro huchaganyikiwa kwani yaliyo katika intaneti na
mitandao ya kijamii huwa tofauti na uhalisia wa mambo katika jamii ya kawaida.
Baadhi ya mabarobaro hushindwa kudhibiti hisia zao, wengine huwa na hasira na
kwa ujumla kukosa uthabiti wa kihisia.
Watoto na mabarobaro
ambao hutegemea sana intaneti na mitandao ya kijamii hatimaye hukumbwa na
uraibu kutokana na kutumia wakati wao mwingi wakiwa online. Hii ni katika hali
ambayo wakitumia nishati na wakati wao mwingi katika harakati za kifikra na
ubunifu wanaweza kuboresha vipaji vyao na hivyo kuimarisha uwezo wao wa
kuchagua kazi bora katika siku za usoni.
Kwa mtazamo wa afya ya
kisaikolojia ustawi wa kimaadili katika jamii hutegemea kuwepo uhusiano salama
na endelevu.
Kuna watumizi wa
intaneti ambao hutumia wakati mwingi katika intaneti kujifunza itikadi na
tamaduni batili ambazo baadaye huwaletea madhara. Aidha wengine hutumia wakati
wao mwingi katika intaneti wakiwasiliana na marafiki bandia na wa muda. Iwapo
fursa na kipindi hicho kingetumiwa kuwahudumia watu wa familia, basi jambo hilo
lingekuwa na taathira nzuri katika ustawi wa kimaadili wa mabarobaro.
Uhusiano bora wa
kifamilia huimarisha kina cha mshikamano baina ya jamaa. Mabarobaro wanapaswa
kukumbuka ukweli kuwa, jamaa katika familia ni watu wanaoweza kuaminika zaidi
kwani zaidi ya wengine wote, wao huwa wanamjali barobaro mbali na kufurahi
anapopata ufanisi na mafanikio maishani.
La kusikitisha ni kuwa
barobaro huyo leo amezama katika vivutio bandia vya ulimwengu wa intaneti na
mitandao ya kijamii na hivyo kujitenga na ulimwengu wa kawaida sambamba na
kupoteza ujuzi wa kuanzisha uhusiano wa kijamii na watu anaoishi nao katika
familia au jamii. Ni kwa sababu hii ndio kadiri siku zinavyosonga mbele yeye
hutumbukia katika kinamasi cha ulimwengu wa intaneti. Pasina yeye kutafakari ni
kipi kinachomfanya akumbwe na mfadhaiko wa nafasi na kumuweka mbali na ile
furaha ya kuwa na uhusiano wa kihisia na wanadamu wengine, yeye huwa anajaribu
kuanika picha zake mbali mbali katika intaneti sambamba na kuelezea harakati
zake za kimaisha kwa marafiki wa intaneti ili aweze kuwavutia. Hii ni katika
hali ambayo anajua vizuri sana kuwa marafiki wa intaneti wanaodai kumpenda au
wanaomshangilia hawafanyi hivyo kwa dhati ya moyo.
Nukta nyingine hapa ni
kuhusu kutafuta marafiki wa kiintaneti kupitia mitandao ya kijamii, kumbi za
mazungumzo au chat rooms au kubonyeza mitandao ya ufasiki na iliyo dhidi ya
thamani za kidini. Hayo ni mambo ambayo huwa na taathira mbaya sana kwa watoto
na mabarobaro kwa mtazamo wa kijinsia, kifikra na kidini.
Wasichana na wavulana
mabarobaro wanaotembelea mitandao ya kijamii katika intaneti aghalabu hufanya
hivyo pasina kuhusisha wazee au familia zao. Wao hujuana na kuanzisha uhusiano
kwa njia ya intaneti na mitandao ya kijamii.
Uhusiano na maingiliano
katika ulimwengu wa kawaida huwa na ugumu kutokana na kuogopa wazazi au kuhofia
kuaibika na kufedheheka. Imeshuhudiwa mara nyingi namna watu wahalifu
wanavyoibua akaunti bandia na kuingia katika mitandao ya kijamii yenye
mabarobaro wenye msisimko mkubwa. Wakiwa hapo huanza kuwatumia vibaya
mabarobaro na watoto ambao bado hawajapevuka kiakili na ambao huamini kila
wanachoambiwa. Yanayojiri baada ya hapo wakati mwingine huwa ya kusikitisha
sana. Katika baadhi ya mitandao ya kijamii kuna picha na video nyingi zilizo
kinyume cha maadili. Picha hizo za ufuska huingizwa katika mitandao ya kijamii
na intaneti pasina kuwepo udhibiti wa aina yoyote. Picha hizo za ufuska na
ponografia huathiri vibaya akili za watoto na mabarobaro na kuwasababishia
matatizo mengi kama vile kubaleghe haraka.
Taswira hizo za kifasiki
hujikariri mara kwa mara katika ubongo wa waliozitazama na kadiri muda
unavyosonga mbele, ile hali ya watoto na mabarobaro kuwa na haya huondoka.
Hakuna shaka kuonyeshwa na kusambazwa picha za ngono katika intaneti huwa na
taathira mbaya sana katika uhusiano baina ya watu. Hali kama hiyo hupelekea
kuenea uhusiano haramu wa kijinsia ulio nje ya mafundisho ya kidini, mila, ada
na desturi za jamii.
Kama tulivoona awali
utumizi mbaya wa intaneti na mitandao ya kijamii huathiri vibaya malezi bora ya
watoto na mabarobaro ambao kwa hakika ni mustakabali wa jamii. Weledi wa mambo
wamebaini kuwa wakati mwingine kutokana na kuwa wazazi nao wana utovu wa maadili
na ni waraibu wa intaneti, mabarobaro nao huwaiga wazazi wao. Kwa hivyo
kutokuwepo kigezo bora hupelekea mabarobaro watumbukie katika mkondo potovu.
Kwa kuzingatia kuwa intaneti na mitandao ya kijamii haitumiwi tu na mabarobaro
na vijana, watu wazima wanaotumia teknolojia hii pia nao wanapaswa kuwa
waangalifu. Leo watu wazima pia hutumia wakati wao mwingi wakiwa katika
intaneti na mitandao ya kijamii kuwasiliana na jamaa na marafiki. Iwapo
tunataka kutoa mtazamo wa kiadilifu, tunaweza kusema kuwa teknolojia za
kisasa za habari na mawasiliano au technohama imekuwa na nukta zake nzuri na
chanya katika jamii ya mwanadamu. Lakini kile ambacho kinapelekea intaneti na
mitandao ya kijamii kuwa na madhara ni namna inavyotumiwa. Kimsingi ni kuwa
iwapo mwanadamu ataondoka katika mkondo wa wastani katika chochote kile
anachofanya, basi yamkini hilo likaambatana na hasara au madhara. Hili ni kweli
pia katika utumizi wa mitandao ya kijamii.
Technohama imekuwa na
nafasi kubwa katika kurahisisha na kuboresha maisha ya mwanadamu katika dunia
ya leo. Kwa kustawi sayansi na teknolojia matatizo mengi kama vile maradhi
hatari yameangamizwa katika jamii ya mwanadamu.
Ingawa miaka ya nyumba
masafa yalikuwa na taathira katika uhusiano na maingiliano ya wanadamu, leo
mawasiliano ya wanadamu yameenea na kuwa na kasi ya juu kutokana na kuenea
intaneti na mitandao ya kijamii katika kila kona ya dunia.
Katika miaka ya nyuma,
iwapo mtu aliyeishi katika nchi nyingine angetaka kuwasiliana na jamii au
familia, njia pekee ya haraka ilikuwa ni kutumia simu ambayo iligharimu kiasi
kikubwa cha fedha. Lakini leo tunashuhudia kuwa, watu walio katika maeneo
tafauti ya umbali wa maelfu ya kilomita wanawasiliana kwa kasi ya sekunde
chache tu tena kwa gharama ya chini kabisa na hata wakati mwingine pasina
kutoa malipo kwa kutumia mitandao ya kijamii.
0 comments:
Post a Comment