Random Post

Thursday, March 17, 2016

Food Poisoning (Kudhuriwa na chakula)


Food Poisoning (Kudhuriwa na chakula)


Wapenzi  wasomaji karibuni katika kipindi kingine cha Ijue Afya Yako. Kipindi ambacho lengo lake ni kujadili masuala mbalimbali yanayohusu afya na tiba ili kupata ufahamu zaidi juu ya kuimarisha afya zetu na ya jamii nzima kwa ujumla. Hii ni sehemu nyingine ya makala ya Ijue Afya Yako, ambapo tutazungumzia sumu inayopatikana ndani ya vyakula au kwa kimombo food poisoning, karibuni.
&&&&&&&&&&
Neno food poisoning au kudhuriwa na chakula ni tatizo linalotokea baada ya kula chakula au kunywa kinywaji kilichochanganyika na vijidudu au kitu chenye sumu au kuguswa na aidha sumu za bakteria na vimelea vinginevyo vya maradhi. Kwa ujumla hali hii hutokea baada ya mtu kula chakula kulichochafuliwa na matokeo ya hali hiyo ni mtu kupatwa na maumivu ya tumbo, tumbo kukata, kuharisha, kutapika na dalili nyinginezo. Kesi nyingi za kuchafuliwa huko kwa chakula zinatokana na ulaji wa vyakula vilivyochafuliwa na bakteria wenye kusababisha madhara. Hata hivyo food poisoning inaweza pia kusababishwa na virusi, kemikali, mimea na samaki wenye sumu. Kwa kawaida mazingira anayoishi binadamu yamezungukwa na vijidudu katika kila kona, kwa hiyo kutokea uchafuzi wa chakula ni jambo la kawaida huku baadhi ya vimelea hao pia wakiwa na manufaa kwa mazingira na pia binadamu. Tatizo la sumu inayotokana na chakula baadhi ya wakati hutishia maisha ya watu, na nchini Marekani pekee maisha ya mamilioni ya watu huwa hatarini kila mwaka kutokana na food poisoning.
Tatizo la food poisoning linaweza kusababishwa na vitu vifuatavyo:-
1. Bacteria: Campylobacter ndio bakteria wanaosababisha sumu kwenye vyakula kwa kiasi kikubwa na kumpelekea muathirika kuharisha. Bakteria huyo kwa kawaida hupatikana katika vyakula, maji au maziwa yasiyochemshwa na pia kupitia wanyama walioathirika. Bakteria wengine wanaosababisha tatizo hili ni Salmonella, E. coli, Shigella na aina ya Clostridia.
2. Parasite (vimelea): Amoeba na giardia pia huleta matatizo kwenye chakula. Vimelea hawa wanapatikana kwa kiasi kikubwa katika nchi zinazoendelea.
3. Virusi: Baadhi ya virusi kama rotavirus pia huleta matatizo kwenye chakula
4. Sumu au kemikali: Baadhi ya bakteria wanaweza kuchafua chakula hivyo kinapoliwa huleta madhara. Samaki kama tuna wana kiasi kikubwa cha madini ya zebaki au mercury hivyo wakiliwa na mama mjamzito huleta madhara kwa mtoto aliye tumboni. Vimelea hao wanaotuzunguka wanapatikana pia kwenye chakula na wakati mwingine wanaweza kuwa wa manufaa kwetu. Hata hivyo bakteria ambao wako katika vitu vilivyooza na mabaki ya vyakula, pia huleta madhara.
Lakini je chakula kinaweza kuchafuliwaje?
Chakula kinaweza kuchafuliwa wakati wa uzalishaji, kuhifadhiwa au kupikwa. Kwa mfano kutohifadhi chakula kwa usahihi au kwenye joto lililosahihi kama kutoweka chakula kwenye jokofu. Tatizo hili hutokea sana kwa vyakula vya jamii ya nyama, maziwa na samaki. Pia kutopika chakula sawasawa. Mara nyingi bakteria huwepo katika nyama mbichi hivyo isipopikwa na kuiva vizuri huweza kuleta madhara. Chakula pia kinaweza kuchafuliwa pale mwandaaji wa chakula asipofuata kanuni za afya na usafi. Maji pia yanaweza kuwa machafu pale bakteria au kinyesi cha binadamu na wanyama kinapoingia au kuchanganyika na maji. Tatizo hili hushuhudiwa sana katika nchi na mazingira yenye usafi duni. Katika nchi kama hizo, chakula pia kinaweza kutengenezwa ama kutayarishwa kwa kutumia maji yenye vimelea. Vyakula vinavyotokana na wanyama, vyakula vibichi na vile vya jamii ya mboga ambavyo havioshwi vyema, vyote vinaweza kuwa na vidudu maradhi na kuchafua chakula au kusababisha food poisoning. Backeria kama vile Salmonela na Listeria ni miongoni mwa vimelea vinavyopatikana katika vyakula vilivyoharibika au kuoza.
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
Mtu aliyekula chakula kilichochafuliwa au kugusana na vijidudu maradhi hao huwa na dalili kuu zifuatazo: Kutapika, kuharisha, kichefuchefu na maumivu ya tumbo hali ambayo kitaalamu hujulikana kama stomach flu. Dalili kubwa ni kuharisha na wakati mwingine kutapika na tumbo kusokota. Maumivu hupungua kwa muda hasa baada ya kupata choo. Aidha dalili hizo mara nyingi huambatana na maumivu ya misuli, homa, kutetemeka mwili na kuhisi kuchoka. Hatua ya kuhara na kutapika muathirika husaidia mwili kuondoa mada zenye sumu au athari katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula (digestive tract) na hivyo kuzizuia sumu au vijidudu maradhi hivyo kuingia katika mfumo wa damu. Wakati mwingine inakuwa vigumu kueleza iwapo umepatwa na tatizo la food poisoning baada ya kula chakula kilichoharibika. Hivyo iwapo mtu atakuwa na mojawapo ya dalili hizo zilizotajwa, kama vile tumbo kukata na kuharisha ni vyema awaulize watu wengine wa familia iwapo kuna wengine walio na dalili kama hiyo na kama wamekula chakula kama hicho alichokula yeye. Wakati mwingine mtu huanza kujisikia mgonjwa katika muda wa masaa machache baada ya kula chakula kilichochafuliwa na sumu za bakteria au na vimelea maradhi. Dalili huanza kujitokeza kuanzia muda wa saa moja hadi matatu baada ya kula chakula kisichofaa. Pia wakati mwingine mtu huwa hahisi kuwa mgonjwa, hadi kupita siku kadhaa baadaye na iwapo mtu atakuwa amekula chakula kilicho na kiasi kidogo cha sumu muda wake wa kuuugua utakuwa mfupi na mara moja ataanza kujisikia vizuri. Katika hali kama hiyo mtu anapoona ana dalili hizo tulizozitaja, ni vyema amuone daktari mapema kwa ajili ya matibabu. Iwapo utakwenda kwa daktari atakuuliza maswali mengi kama vile unajisikiaje, umeanza kuumwa lini, ulikula nini hapo kabla na kama kuna mtu yoyote wa karibu yako aliye na dalili kama zako. Aidha daktari anaweza kukuandikia vipimo vya haja kubwa na ndogo ili kuona kama vijidudu maradhi hivyo ndivyo vimesababisha hali hiyo iliyokusibu au la. Pia iwapo utaona damu ndani ya kinyesi, unashauriwa kumuona daktari mara moja pasina kuchelewa.
&&&&&&&&&

Mambo mengi yanaweza kufanywa ili kuzuia vijidudu maradhi na sumu kuchafua chakula chetu. Mosi ni kusafisha vyema mikono kabla na kila mara unapotayarisha chakula na kabla ya kula, na kusafisha sehemu zote zinazotumiwa wakati wa maandalizi ya chakula. Pia madodoki na sponji za kuoshea vyombo kwa kiasi kikubwa huwa na uwezekano wa kubeba bakteria hivyo ni lazima vifaa hivyo vioshwe mara kwa mara baada ya kutumika. Vilevile tunapaswa kufunika kwa sashi au bandage sehemu yoyote yenye mchubuko au uliojikata katika mkono kabla ya kuanza kuandaa chakula. Vyakula aina ya nyama na mayai vinapaswa kupikwa vyema na kupashwa moto vizuri kabla ya kuliwa. Pia tuhakikishe kwamba majokofu au mafriji yanakuwa katika nyuzi joto 40 na freeza katika nyuzi 0 au chini ya hapo ili kuhakikisha kwamba vyakula vinahifadhiwa vyema na kuepusha muozo. Kiporo cha chakula kisikae ndani ya jokofu kwa zaidi ya siku nne, nyama haipaswi kuachwa ovyo bila ya kuhifadhiwa, na ni vyema ichemshwe kwa zaidi ya nyuzi joto 140. Pia tunapaswa kuwa waangalifu wakati wa kuhifadhi vyakula kama vile samaki na nyama mbichi kwani vinaweza kuchafuliwa kirahisi na bakteria au vimelea wa maradhi. Ni bora samaki wasivuliwe kutoka kwenye maji yaliyochafuka, na tunashauriwa kusafisha mboga mbichi na matunda kabla ya kula au kupika, na pale tunaponunua vyakula vinavyohifadhiwa ndani ya makopo, mikebe na kadhalika tunapaswa kwanza kuangalia muda wa matumizi yake unakwisha lini. Pia vyakula ambavyo vinahifadhiwa katika makopo kama vile samaki, nyama na vinginevyo tunashauriwa kuvichemsha kabla ya kuliwa na pale tunapoona kuwa makopo hayo yamefura kuliko kawaida, hiyo ni dalili kuwa vyakula hivyo vimeharibika. Hii ni kwa sababu bakteria aina ya Clostridium Botulinum anayepatikana katika vyakula vinavyosindikwa katika makopo huweza kusababisha aina ya food poisoning inayotokana na sumu ya botulism ambayo ni hatari na huua. Pia maziwa ya ng'ombe ambayo hayajapitia katika njia ya kuondolewa vijidudu inayojulikana kama pasteurization, yanapaswa kuchemshwa vizuri kabla ya kutumiwa. Itakumbukwa kuwa watoto, wazee na wale wote wenye magonjwa ya muda mrefu au wenye kinga dhaifu ya mwili huwa na hali mbaya wanapokula chakula kilichoharibika au kuchafuliwa na vimelea vya maradhi. Kwa hiyo ili kukabiliana na tatizo hili, tunapaswa kuwa makini sana kuhusiana na suala hili.

0 comments:

Post a Comment